MUUNDO WA MTIHANI WA KISWAHILI


021 KISWAHILI
(Kwa Watahiniwa Walioko na Wasiokuwa Shuleni)
1.0 UTANGULIZI
Fomati hii ya mtihani imetokana na marekebisho yaliyo fanywa katikafomati ya mwaka 2008 iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania. Fomati hii inazingatia muhtasari wa somo la Kiswahili wa mwaka 2010. Maboresho ya fomati yaliyofanyika yamelenga upimaji wa umahiri
unaozingatia viwango vya juu vya kufikiri na hakuna mabadiliko katika mada zitakazopimwa.

2.0 MALENGO YA JUMLA
Malengo ya jumla ya mtihani ni kupima kwa kiwango gani mtahiniwaanaweza:
2.1 kuwasiliana kwa Kiswahili fasaha katika fani mbalimbali za maisha;
2.2 kubaini viashiria vya uthamini wa kiswahili kama sehemu muhimu ya utamaduni wa                   Tanzania                                
2.3 kuonesha ujuzi wa kudadisi na kubuni masuala mbalimbali ya lugha na fasihi ya Kiswahili;
2.4 kutumia kazi za fasihi katika maisha ya kila siku;
2.5 kutumia lugha ya Kiswahili katika miktadha mbalimbali;
2.6 kubainisha njia mbalimbali za ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili ili kiweze kutumika kwa                      mawasiliano na nchi jirani na kimataifa;
2.7 kujisomea maandiko mbalimbali ya Kiswahili;
2.8 kujenga msingi bora na imara wa kujifunza na kujiendeleza; na
2.9 kutumia Kiswahili kupata maarifa, mwelekeo na stadi za kijamii, kitamaduni, kiteknolojia na   kitaaluma kutoka ndani na nje ya nchi.

3.0 UJUZI WA JUMLA
Utahini kwa kutumia fomati hii utazingatia upimaji wa ujuzi na utendaji wamtahiniwa katika:
3.1 kusikiliza na kuwasiliana kwa Kiswahili sanifu katika miktadha mbalimbali;
3.2 kubaini viashiria vya uthamani wa Kiswahili kama lugha ya Taifa;
3.3 kusoma maandiko mbalimbali ya Kiswahili kwa ufanisi;
3.4 kuandika habari fupi na ndefu kwa Kiswahili sanifu;
3.5 kusoma kwa ufahamu na kujisomea ili kupata maarifa na kwa burudani;
3.6 kutumia lugha ya kifasihi katika mawasiliano kwa kuzingatia stadi zote za lugha na;
3.7 kutafiti vipengele mbalimbali vya lugha ya Kiswahili.

4.0 MAELEKEZO YA MTIHANI
Mtihani wa somo la Kiswahili utafanywa kwa muda wa saa tatu (3). Mtihani utakuwa na karatasi moja (1) iliyogawanyika katika sehemu A, B na C zenye jumla ya maswali 12. Mtahiniwa atatakiwa kujibu jumla ya maswali 11 yenye jumla ya alama 100.

Sehemu A itakuwa na maswali mawili (2). Swali la kwanza litakuwa la kuchagua na litakuwa na jumla ya alama 10. Swali la pili litakuwa la kuoanisha na litakuwa na jumla ya alama 5. Mtahiniwa atatakiwa kujibumaswali yote. Sehemu hii itakuwa na jumla ya alama 15.

Sehemu B itakuwa na maswali sita (6) ya majibu mafupi. Swali la 3 na 4 yatakuwa na alama nne (4) kwa kila moja ambapo swali la 5 - 8 yatakuwa na alama nane (8) kwa kila moja. Mtahiniwa atatakiwa kujibu maswali yote. Sehemu hii itakuwa na jumla ya alama 40.
Sehemu C itakuwa na jumla ya maswali manne (4) ya insha. Mtahiniwa atatakiwa kujibu maswali matatu (3). Sehemu hii itakuwa na jumla ya alama 45.

5.0 MADA ZA KUTAHINI
5.1 Ufahamu
5.2 Sarufi
5.3 Utumizi wa Lugha
5.4 Uandishi
5.5 Maendeleo ya Kiswahili
5.6 Fasihi

Tanbihi
Orodha ya vitabu vya Fasihi vitakavyotumika katika somo la Kiswahili ni
vilivyoidhinishwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.