mwisho wa ubaya aibu
na
aziza a. zaburi
SHUKRANI
Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu (Allah(s.w))
muumba na muweza wa kila kitu, kwa kunijaalia afya njema, nguvu, uwezo, akili,
busara, maarifa, utulivu na uvumilivu katika kipindi chote cha masomo yangu.
Namshukuru tena kwa unyenyekevu pamoja na tauhidi kwa kusema, Alhamdulillah
Rabbil 'alamin.
Pili,
napenda kumshukuru kwa dhati kabisa, mwalimu wangu wa somo la Kiswahili kwa
kuniongoza vyema katika kila hatua kuandika kitabu hiki. Hakusita wala
hakuchoka kunishauri na kunirekebisha namna ya kuandika vitabu ikapelekea
kukamilisha kuandika kitabu hiki. Amenilea kitaaluma pamoja na kunifunza
misingi ya nadharia za fasihi, fasihi fafanuzi na mbinu za uandishi wa vitabu
ambazo zimezaa kazi hii. Namuomba Mwenyezi Mungu ambariki na ampe afya njema
pamoja na ukakamavu na amzidishie kila la kheri, na kumuepusha na kila la
shari, Amin.
Tatu,
napenda kuishukuru familia yangu kwa uvumilivu waliouonyesha kwa kuelewa kuwa
nilikuwa nafanya kazi ya shule, kwani kwa baadhi ya nyakati walikosa kunitumia
katika kazi mbalimbali za nyumbani wakanipa muda ili nikamilishe kazi hii.
Nne,
napenda kuwashukuru walimu wangu wa shule ya sekondari Engusero kwa kunilea
kitaaluma na kunikuza kinadharia na vitendo. Walimu hao ni pamoja na Mkuu wa
shule, Makamu mkuu wa shule, Mtaaluma na waalimu wengine wote wa shule ya
sekondari Engusero.
TABARUKU
Natabaruku
kazi hii kwa wazazi wangu, Bw. Athumani Zaburi na Bibi Amina Omari kwa kunizaa,
kunilea, kunisomesha, kunifunza mema, kunikataza mabaya, na kunipa moyo na
kuniwezesha kifkira na maadili mema katika kipindi chote cha masomo yangu,
tangu darasa la kwanza mpaka sasa kidato cha sita. Mawazo yao na busara zao
katika elimu nitazikumbuka daima na kuwa chachu ya kujiendeleza zaidi.
Vilevile
ninawatabarukia kaka zangu Bashumu Athumani na Shiraji Athumani, kwa ushawishi,
uvumilivu, huruma na kunitia moyo pale nilipokata tamaa katika masomo yangu
mpaka leo nafikia kidato cha sita. Pia kwa msaada wa hali na mali katika
kukamilisha kazi yangu hii, ikiwa ni pamoja na gharama za masomo na kuwa wasimamizi
na nguzo imara na thabiti katika kuhakikisha sikati tamaa ila ninamaliza masomo
yangu, tangu kidato cha nne mpaka leo kidato cha sita
KAZI
HII INAPATIKANA PIA KATIKA TOVUTI IFUATAYO
BARUA
PEPE: alfanizaboori@gmail.com
Shukurani
zote njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu (Allah (s.w)) aliye Bwana na Mlezi wa
walimwengu wote.
Ninamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuniwafikisha kutoa kitabu hiki MWISHO WA UBAYA AIBU kama
muendelezo wa kazi za kitaaluma katika somo la Kiswahili baada ya kutoa kitabu
cha kwanza UZAZI WA MSOTO.
Lengo la kitabu
hiki ni kuelimisha jamii juu ya matatizo wanayoyapata watoto yatima na wajane
(wanawake waliofiwa na waume zao) kama vile:-
(i)
Mke na watoto kufukuzwa katika majumba
wanayoishi na Ndugu wa marehemu
(ii)
Watoto kukatisha masomo
(iii)
Kufanyiwa vitendo vya kikatili kama vile
kubakwa na unyanyasaji wa kijinsia
(iv)
Kuzuka kwa ajira za utotoni
Wito wa
mwandishi kwa jamii nzima, ni kuwatunza mayatima na wajane ni jukumu la jamii
nzima kwani na yeye alikua na wazazi kama wewe naye alikua na mume kama wewe
mwanamke uliye na mume.
SEHEMU YA KWANZA
Tina alikuwa amelala kifudifudi
kitandani pake akilia kwa majuto na upweke alioachiwa na mume wake kipenzi
bwana Alfan. Zaidi ni yule mtoto aliyeachwa na baba yake yungali mdogo kila
alipomwangalia mtoto wake huzuni na majonzi yalimtanda kwenye akili yake lile
tumaini lote alilokuwa nalo lilitoweka ghafla Tina aliurejea upweke wake ambao
aliachiwa na wazazi wake pale tu mume wake alipoaga dunia kwani mume wake
alikuwa ni tegemezi lake la mwisho baada ya wazazi wake kupoteza maisha kwa
ajali ya moto bwana alfani alikuwa ni msaada mkubwa kwa Tina alimpenda na
alimthamin na kumpa heshima ya hali ya juu, bwana Alfani alikuwa na sifa za
kipekee ambazo wanaume wengi wa kijiji chao hawakuwanazo, Tina alijivunia sana
mume wake, lakini furaha yote ilipotea pale tu bwana Alfani alipoaga dunia Tina
alijihisi ni mgeni wakati yupo kwenye nyumba yake alipambana na maswali magumu
ambayo aliulizwa na mtoto wake aliyeitwa Chiku mara kwa mara, Chiku alikuwa ni
mtoto mwenye umri wa miaka sita alipedwa sana na marehemu baba yake, alikuwa ni
mtoto wa Darasa la kwanza kila alipo kwenda shule baba yake alimsindikiza kwa
baiskeli huku akimsimulia hadith ambazo kila mtoto alizipenda, bwana Alfani
alikuwa na upendo wa dhat kwa familia yake ambao ulimvutia kila mwanamke.
Siku moja Tina na mwanawe walikuwa
wameketi kwenye mkeka, huku akimsimulia hadithi ambazo alikuwa akisimuliwa na
baba yake, lakini Chiku alionekana kuto kuwa na furaha, alimuuliza mama yake,
mama baba yuko wapi? Tina alionesha kuto kumzingatia Chiku, Chiku alimuuliza
tena mama yake, mama! Baba Yuko wapi? Tina akamwambia Chiku, mwanangu baba
ameenda mjini atarudi kesho, hapana mama! Baba hatorudi kwa sababu watu
wanasema baba amekufa! Chiku aliongea huku anabubujikwa na machozi Tina
hakuelewa nini cha kumjibu mototo wake, alitokwa na machozi kisha akasema ,
mwanangu Chiku hao ni waongo, waongo? Hapana mama ni kweli, sasa nani atakaenipeleka
shule? Nani atakae nisimulia hadithi za sungura na fisi? Mama niambie basi! Niambie
mama yangu, Tina alimkumbatia mwanawe kisha akasema, mwanangu niamini mimi mama
yako, wakati Tina anamliwaza Chiku, mlango uligongwa, ngo! ngo! ngo! Tina na
Chiku walishtuka, mlango uligogwa tena, ngo! ngo! ngo!, Tina alinyanyuka
akaenda Kufungua mlango alipofungua mlango, alikalibishwa na sura za watu
wawili zimekunja kama sura za vikongwe, ilhali wao ni vijana, Tina aliwakaribisha
kwa furaha, lakini cha ajabu wageni wale hawakujibu chochote wakaingia ndani
wakaketi kwenye viti Chiku alielekea kule waliko wageni kisha akawasalimia,
shikamoo baba mdogo, shikamoo baba mkubwa, wawili wale waliangaliana kisha
wakaitikia kwa pamoja marahaba, Chiku aliendelea kwa kusema, eti baba anarudi
lini? Baba yako?, Mmoja kati ya wawili wale aliyejulikana kwa jina la Kangomba
alishangaa! Mwingine akaropoka Kwa kusema baba yako amekufa, Tina alidakia kwa
kusema shemeji nini unamwambia mtoto? Hujui Kama……………………, Chiku aliangua kilio
akamwambia mama yake, mama kumbe ni kweli baba amekufa? Tina alichukizwa na
kitendo walichokifanya shemeji zake, lakini hakuwaonesha ni jinsi gani amechukia,
akamnyanyanyua chiku kisha akasema mmewaacha wazima wote huko nyumbani?
Kangomba akajibu, hatuhitaji salamu wala maongezi na wewe, ila tumekuja kwa
ajili ya jambo moja tu, Kama bwana Alfani amesha kufa sasa unasubili nini
kwenye nyumba hii, Jua kabisa kwamba hii nyumba si yako wala si ya alfani,
tunaomba uchukue kilicho chako uondoke. Tina alihamaki kisha akasema siondoki
nitabakia hapahapa, mnaponiambia niondoke na huyu mtoto ataishije? Na mimi
nitaenda wapi? Utaenda wapi, Kabla haujaolewa na alfani ulikuwa unaishi wap? Mwingine
kati ya wawili wale akasema kwa hiyo ulimroga Ndugu yetu ili urithi nyumba? Tina
alilia huku anasema mbona hamna huruma hata kwa mtoto ambae ni damu ya Ndugu
yenu? Tena nyamaza! Kangomba alipayuka tunavyo fahamu sisi Ndugu yetu hakuwa na
uwezo wa kupata mtoto! Mh! Tina alipigwa na butwaa akasema kama Ndugu yenu
hakukuwa na uwezo wa kupata mtoto sasa huyu mtoto ni wanani? Kwani nani asiye
fahamu hapa kijijini kama wewe ni kahaba, Malaya, mzinzi, nani asiyejua si
nakuuliza? usitucheleweshee muda wetu chukua kilicho chako ondoka, Kangomba
aliingia chumbani akakusanya mabegi ya
Tina akayarusha nje akamzoazoa Tina na mwanawe chiku akawasukumiza nje, Tina
alimuangalia mtoto wake akalia kwa uchungu na Chiku nae alipomuona mama yake analia
na yeye akaanza kulia, Tina alipiga moyo konde akanyanyua mabegi yake moja
akaliweka kichwani linguine mkononi na Chiku akambeba mgongoni kisha akasema
ama kweli DUNIA HADAA ULIMWENGU SHUJAA, leo hii mimi nafukuzwa kama mbwa,
naambiwa nimemroga mume wangu, alilia sana lakini hakuna aliyemsikiliza,
kangomba na kaka yake walifunga mlango
kisha hao wakaondoka, wakamuacha Tina amechoka haelewi wapi kwa kwenda, baada ya
dakika kadhaa na Tina nae akaondoka
Tina
na mtoto wake Chiku wapo njiani, Tina haelewi aelekee wapi, hana wazazi wala
walezi ambao wataweza kumsaidia lakini aliwaza akajisemea kimoyomoyo, mmh!
Nikiondoka mbali na kijiji hichi mwanangu hatosoma sasa nifanyeje? Aah! Mungu
wangu naomba unisaidie mimi sina kwa kwenda, wala kwa kukimbilia, lakini
alifikiria akaona aende kwanza akamuone wmalimu mkuu wa shule ambayo Chiku
anasoma labda atamsaidia kwa namna moja ama nyingine. Bila kupoteza muda
alimshika Chiku mkono na begi lake moja kichwani jengine mgongoni moja kwa moja
hadi shuleni, alipofika alikuta ofisi imefungwa. Chiku alimwuliza mama yake,
mama! umekuja kuniombea ruhusa? Tina alimfaiji mwanawe kwa kusema ndio
mwanangu, ila leo si juma pili? Chiku alimuuliza mama yake, Tina alivunjika
moyo kisha akamwambia mtoto wake, Chiku tuondoke mwanangu ofisi ya mwalimu
imefungwa. Mama mimi nimechoka kutembea, nabaki hapa hapa nenda kamwambie baba
anifuate na baiskeli, mwanangu Chiku njoo nikubebe mgongoni alafu baba
atatukuta njiani, Chiku alikataa kata kata kisha akamwambia mama yake, mimi
sitaki kuondoka nabaki hapa hapa hadi baba aje. Wakati Tina anaendelea
kumbembeleza mtoto wake, kuna mwalimu alikua anaishi karibu na shule
aliyejulikana kwa jina la mwalimu Doka, alikua anatembelea maeneo ya shule
lakini aliona kama kuna watu wameketi kwenye benchi lililopo mbele ya ofisi ya
mwalimu mkuu, akaelekea kule kule walipokua wamekaa, alipofika pale alishangaa
kumwona Chiku na mama yake wamekaa na wote wana huzuni wa hali ya juu. Mama chiku,
vipi mbona upo hapa ilihali leo ni Juma pili na mbona una mabegi makubwa hivi
unaenda wapi? Mwalimu doka aliuliza, Chiku alikua amepitiwa na usingizi
palepale, mama Chiku alimjibu mwalimu kwa upole, Ah! Mwalimu nahitaji ruhusa kidogo
ya mwanangu hatohudhuria shule kwa siku kadhaa mambo yakikaa vizuri atahudhuria
kama kawaida, mwalimu Doka alimuuliza unakwenda wapi? Tina alimjibu, sina kwa
kwenda kaka yangu, natafuta nyumba nipange, alafu nitafute kazi ambayo
itaniingizia fedha ili niweze kupata fedha ya kumlipa mwenyenyumba, Doka
alishangaa akamuuliza tena unataka kupanga? Kwani nyumba uliyokua unaishi na
marehemu mume wako haikua yakwenu? Tina aliangusha kilio mithili ya mtoto
mchanga mwenye njaa, Mwalimu Doka akajitahidi kumnyamazisha Tina, kisha
akamwinua akamwambia twende nyumbani kwangu ukapumzike kwanza Mwalimu Doka
alimnyanyua Chiku akamweka begani kwake akabeba begi moja la nguo na jingine
akalibeba Tina wakaelekea nyumbani kwa mwalimu Yule, walipofika mke wake
aliwakaribisha wakaingia ndani, mwalimu Doka alimwamuru mkewe amchukue Chiku
akamlaze chumabni, akamkaribisha Tina, nae akaketi kwenye kochi lililotandikwa
kwa vitambaa vizuri vyenye rangi nyekundu yenye kumelemeta, mke wa mwalimu Doka
alimkaribisha mama Chiku kwa glasi ya
juisi ya matunda. Kisha akamwambia jisikie upo nyumbani, kisha akamuomba mumewe
waingie chumbani mara moja, walipofika tu! Mwalimu Doka alishangaa kumuona mke
wake amevimba kama boko aliyeshiba maji ya mto, akamuuliza kuna shida gani? Mbona
si kawaida yako kuwa hivyo? Mume wangu niambie yule mwanamke ni nani yako? Bite
alimuuliza mune wake,kabla mumewe hajajibu akaendelea kwa kusema, mume wangu
ujue mimi nakupenda sana sihitaji nikupoteze, hata mimi nakupenda mke wangu na
sihitaji kukupoteza, na kuhusu Yule mwanamke usiwe na shaka kabisa, kuwa na
amani ndani ya moyo wako mwalimu Doka alimwambia mkewe. Bite alinyanyuka
akamkumbatia mume wake kisha akamwambia wasiwasi ndio akili na ni lazima niwe
na wivu juu yako kwa sababu nakupenda saana, mwalimu Doka alitabasamu kisha
akamwambia, kumbe nawe unawivu kiasi hicho? Usiwe na wasiwasi mimi ni wako
daima, Bite alifurahi kwa maneno mazuri aliyopewa na mumewe, baada ya muda
mchache Bite aliandaa chakula kwa ajili ya wageni na muda ule ule Chiku nae
akaamka alishangaa kuona yupo peke yake kitandani akaita kwa sauti kali mamaaa! Bite aliwahi
chumbani akamnyanyua Chiku akamwambia usilie mtoto mzuri twende kwa mama, Tina
alifurahi kumuona bite alivyokuwa na upendo na ukarimu usio na kifani, mwalimu
Doka nae alifurahi kuona mke wake anawajali wageni, Chiku aliangalia mbele yake
akamuona mama yake na mwalimu Doka wameketi, moja kwa moja alienda kwa mama
yake akamuuliza, kwa nini tupo hapa? Tina alimwambia Chiku amsalimie kwanza mwalimu
wake akamsalimia kisha akaendelea kumuuliza mama yake, mama! tumekuja kufanya
nini hapa? mwalimu Doka alimuita, Chiku akamwambia subiri ule chakula alafu
mama atakujibu maswali yako, Chiku alimsikiliza mwalimu wake akaketi kwenye
kochi na chakula nacho kilikwishakuwa tayali, wakala kwa pamoja walipomaliza, Bite
alimchukua Chiku akamuogesha, alipomaliza tu Chiku alipitiwa na usingizi mzito
na mwalimu Doka nae akapata nafasi ya kumuuliza Tina ni kipi kimemsibu, Tina
alieleza yote yaliyompata na yale yote ambayo shemeji zake walivyomfanyia,
mwalimu Doka alihuzunika sana na alimuahidi Tina kuwa atakuwa nae bega kwa bega
katika kuhakikisha kuwa nyumba anaipata.
SEHEMU YA TATU
Mwalimu Doka alipeleka taarifa kwa
mwalimu mkuu juu ya matatizo aliyoyapata Tina rambirambi zilichangishwa kwa
waalimu pamoja na wanafunzi, wakapata jumla ya shiringi laki moja na nusu moja
kwa moja mwalimu doka alimsaidia Tina kutafuta nyumba ya kupangia akafanikiwa
kupata nyumba iliyokuwa pembezoni mwa
shule, vilevile alimuomba mkewe amsaidie Tina vyombo viwili vitatu ambavyo vitaweza kumsaidia na kuna baadhi ya waalimu wengine
walimpatia Tina vitu mbalimbali wengine
walimpa vyombo, wengine walimpa nguo na mwalimu mkuu alimpa kitanda na godoro, lakini
yote haya yalikuwa ni matunda ya mume wake ambae alikuwa na ushirikiano na
wenzie, Tina alimshukuu sana mwalimu Doka na mkewe pamoja na wale wote ambao
wamemsaidia kwa namna moja ama nyingine, Tina alienda kuyaanza maisha mapya, mwalimu
Doka alienda kituo cha polisi kueleza
jambo ambalo tina limempata na uchunguzi ulianza mara moja !,Tina nae hakuwa
nyuma nyuma, alianzisha biashara ya mkaa ambayo ilimpatia fedha za kukidhi
mahitaji yake madogo madogo, watu wote mtaani walimtambua, kutokana na maneno
yake mazuri kwa wateja wake, watu kutoka mitaa mbalimbali walimiminika kwa mama
Chiku kuhitaji mkaa, Tina alifuahi sana na maisha yake yalipiga hatua siku hadi
siku, alimjali sana mtoto wake, alimwamsha mapema kwa ajili ya kuwahi shule, alimpenda
sana mtoto wake kwani yeye alikuwa ndilo tegemeo lake la mwisho na ndugu yake
wa pekee, Chiku nae alikuwa ni mtoto mwenye adabu, heshima na niddamu ya hali
ya juu kwa waalimu wake na mama yake pamoja na watu wote waliomzunguka, waalimu
walimpenda sana Chiku alifanya vizui katika masomo yakeke, kitu ambacho
kilimfanya mama yake awe na furaha muda wote na aone kuwa bado mume wake yu
pamoja na yeye katika kumpa malezi bora mtoto wao wa pekee. Tina hakuishiwana hamu ya kumpa
mwanawe maneno ya kumpa faraja, ambayo yatamsahauisha upweke alioachiwa na baba
yake pamoja na ule ubaya aliofanyiwa na baba zake wadogo.
Ilikuwa ni siku ya kufunga shule, siku
ambayo Chiku alipewa Zawadi kwa kushika nafasi ya kwanza katika Darasa lao, lakini
hakuzifurahia Zawadi zile kwasababu alimkumbuka sana baba yake pale ambapo
alifanya vizuri katika masomo yake alimpeleka sehemu yenye miti mizuri yenye
vivuli vya kuvutia na kuanza kumsimulia hadithi nzuri zenye kuvutia lakini leo
hii alijiuliza ni nani ambae atamfanyia yote yale ambayo baba yake alikuwa akimfanyia aliishia
kububujikwa na machozi alirudi nyumbani hali ya kuwa hana furaha, mama yake alimuuliza ni kitu gani
kinamkosesha furaha, Chiku alianza kulia huku akimpa mama yake ripoti ya matokeo
pamoja na Zawadi alizopewa Tina aligundua kitu, haraka akaingiza ndani makopo
ya mkaa akamchukua chiku wakaelekea sehemu ambayo baba yake alikuwa anampeleka
walipofika Chiku alisahau yote alifurahi sana na kujihisi yupo na baba yake
kipenzi, akamuahidi mama yake kuwa atampenda na atamtunza kadri ya uwezo wake, jua
lilipoanza kuzama Tina na mwamawe
wakaondoka, walipofika nyumbani, Tina aliandaa chakula kizuri kwa ajili ya
mwanawe, na Chiku nae alikifurahia chakula basi furaha ilitanda ndani ya nyumba
ile
SEHEMU YA NNE
Chiku
alipokuwa likizo alimsaidia mama yake kazi ndogondogo, katika muda ule wa
likizo Tina alianzisha mradi wa matunda, Chiku alikuwa anazunguka mitaani kuuza
matunda na mama yake alikuwa anabakia nyumbani anauza mkaa, Chiku alishazoea
maisha ya kuzunguka mtaani ingawa kuna baadhi ya wanafunzi wenzake ambao
walikuwa wanamcheka na kumpa jina la “MTOTO WA MTAANI’’ lakini yeye hakujali kwa sababu alikuwa ana nia ya kumsaidia mama
yake jua, mvua vyote viliishia mwilini mwake, lakini hakuchoka hata siku moja
kila alipoamka asubuhi alichukua beseni lake la matunda na kujichanganya mtaani
, Chiku alikuwa ni mtotpo mdogo wa Darasa la tatu lakini alifanya kazi ambazo
zilikuwa si za kuzifanya yeye ila tu ilimbidi afanye hivyo hivyo, hata Tina nae
hakupenda mtoto wake aishi katika mazingira yale lakini atafanyaje hali ya kuwa
hana uwezo wa kumpa starehe ambazo watoto wengine wanapewa na wazazi wao .
Siku moja Tina na mwanawe Chiku walikuwa
wanakwenda sokoni Kufuata matunda ya biashara, ghafla Tina alimuona shemeji
yake Kangomba, Tina alishtuka akajitahidi kumzuia mtoto wake ili asimuone baba
yake mdogo kwani akimuona atakumbuka machungu ambayo yameshapita, Kangomba
alimwona Tina na mwananawe, akasema, Mmh! Huyu kahaba bado yupo? Inabidi nimpe
taarifa bwana mkubwa ili tumshughulikie aondoke. Tina na Chiku walinunua
matunda wakaondoka. Kangomba
aliwafuatilia nyuma bila ya wao wenyewe kujua akapafahamu wanapoishi, bila
kuchelewa Kangomba alienda kwa kaka yake akamueleza kile alichokiona na akamuambia
kuwa kama wakimuacha Tina aendelee kuishi katika maeneo yale atawasababishia
matatizo, walikubaliana waende kwa Tina wakamfanyie kitu ambacho hatokuja asahau
katika maisha yake, ghafla mlango uligogwa ngo! ngo! ngo! Sunga alinyanyuka
akaenda kufungua mlango, alipofungua akaona watu wanne wamesimama mlangoni, Sunga
aliwauliza niwasaidie nini? Mmoja kati yao akaonesha kitambulisho kisha akasema,
mimi ni askari, unahitajika kituo cha polisi mara moja, huku ndani Kangomba
aliposikia mambo ya askari, akaogopa sana kisha akachungulia dirishani akawaona
watu wanne lakini kati yao alimfahamu mmoja ambae ni mwalimu Doka kwa sababu
alikuwa akimuona kwa kaka yake Alfani wakati wa uhai wake, akaona imesha kuwa
balaa akafungua mlango wa nyuma akakimbia, bwana Sunga alijaribu kuuliza nini
kimetokea lakini aliambiwa ataenda kujua huko huko, askali wawili wakaingia
ndani wakaangaliaangalia hawakufanikiwa kukuta mtu, wakatoka nje wakamchukua
bwana Sunga wakampeleka kituoni,
Kangomba alipofika nyumbani kwake alijiuliza ni kwa nini mwalimu Doka
ameamua kumsaidia Tina lakini akasema ndani ya usiku wa leo lazuma nipoteze
ushahidi wote, akaandaa kikosi cha watu kumi wenye nguvu akawapa fedha na
akawaambia wakamsambaratishe mwalimu Doka wakimaliza wakafanye fujo kwa Tina na
wakiweza wamuue yeye pamoja na mtoto wake, majira ya saa saba usiku walienda moja
kwa moja kwa mwalimu Doka wakaeeneza petroli katika kila pembe ya nyumba ille wakawasha
moto maskini mwalimu Doka na mke wake walijaribu kuokoa maisha yao lakini
walishindwa, moto ulienea nyumba nzima na nyaya za umeme zikadaka moto na
kusababisha shoti ambayo iliwamaliza moja kwa moja, majirani walifanya
jitihada za kuokoa maisha yao lakini
walishindwa, lile kundi la vijana kumi wakiongozwa na Kangomba wakaenda moja
kwa moja hadi kwa Tina mmoja wao akagonga mlango, ngo! ngo! Tima alijikurupua
kitandani, mlango ukagogwa tena, ngo!ngo!ngo! Tina aliuliza kwa uoga ni
na………na…..ni wewe? Yule kijana akajibu ni mimi apa nahitaji mkaa ! mkaa usiku
kama huu? Tina aliuliza tena, ndio dada yangu nina mgojwa anahitaji kula sasa
tumeishiwa na mkaa, Tina aliogopa lakini kutokana na moyo wa huruma aliokuwa
nao akafungua mlango, alipofungua mlango
alishangaa kuona kipande cha mtu
kimesimama mbele yake punde si punde kundi la watu ambao walivalia mavazi meusi
likamvamia wakamfunga kitambaausoni, wakamlaza chini wakamvua nguo wakamuacha
kama alivyozaliwa wakaanza KUMUASI, mmoja baada ya mwingine, Tina alijaribu
kupiga yowe lakini sauti haikutoka kwa sababu walikwisha mfunga kitambaa usoni,
walimfanyia tendo la kinyama kila mmoja alimuingilia anavyotaka, kisha
wakaondoka. Tina alilia sana, akajuta ni kwa nini alizaliwa katika dunia hii,
akaona ameshapoteza thamani katika maisha yake ,akahisi amepoteza heshima yake
yote alitamani afe kuliko kuishi akajalibu kujiinua pale alipolala lakini
alishindwa alihisi maumivu makali katikati ya mapaja yake, damu zilimtoka hadi
akaishiwa na nguvu akapoteza fahamu, kulipopambazuka, Chiku aliamka akashangaa kuona yupo peke yake
kitandani, alidhani kuwa mama yake yupo nje anaendelea na biashara yake ya
mkaa, lakini aliyaona makopo ambayo mama yake anatumia kupimia mkaa, akadhani
kuwa labda atakuwa amefuata matunda sokoni, alipotoka nje alimuona mama yake
yupo uchi na,mwili mzima zimemjaa damu, aliogopa sana akawahi ndani kuchukia
nguo na kwenda kumsitili mama yake alijalibu kumuamsha mama yake lakini
hakuamka. Chiku alilia saana majirani walikimbilia kule alipo Chiku walipofika
wakashangazwa na kile walichokiona bila
kuchelewa wakamuwahisha hospitalini, Chiku alibaki nyumbani wakati hana amani, alilia
sana mpaka sauti ikamuishia, ghafra
mlango uligogwa, ngo !ngo! ngo! Alipotoka nje alimkuta rafiki yake
anaeitwa Emma analia akamuuliza kwa nini unalia? Akamuambia kuna taarifa mbaya
mwalimu Doka na mke wake wamefariki,
wamefariki? Chiku aliuliza kwa mshangao, akadondoka chini akapoteza fahamu, Emma alipiga kelele kwa ajili ya kutaka
msaada, muda uleule kuna mama mmoja alikuwa amekuja kwa mama Chiku kuhitaji
mkaa lakini alimkuta Chiku yupo katika hali mbaya akamuwahisha hospitalini
alipofika alishangaa kuona na Tina nae yupo hospitali ,
Masaa matatu yalipita Tina na mwanawe walikuwa
hawajapata fahamu, majrani walihuzunika sana
kwa kitendo alichofanyiwa Tina
lakini watu walijua moja kwa moja kuwa Kangomba ndie aliyefanya yote na
kuna mmoja wao akasema kuwa ameokota pochi ndani yake kuna vitambulisho vya Kangomba,
taarifa zilifikishwa kituo cha polisi na harakati za kumtafuta zikaanza,Tina na
mwanawe walipata fahamu madaktari wakajitahidi kutoa matibabu kwa wawili wale
hadi wakapona, lakini Tina hakuona tena thamani ya yeye kuendelea kuwa hai pale tu aliposikia kuwa mtu ambae alikuwa ni msaada
mkubwa kwake, aliyemsaidia kupigania haki yake amepoteza maisha, akikumbuka na
ule unyama aliofanyiwa akuona haja ya yeye kuendelea kuishi katika dunia
iliyojaa uozo na uchafu wa kila aina, lakinipia alipata hamu ya kuishi pale
alipomuona Chiku, marafiki zake walijitahidi kuwa karibu nae na kumpa moyo
lakini alihisi bado anadharaulika kwa kile alichofanyiwa, baada ya siku kadhaa
Kangomba alikamatwa akapelekwa kituo cha polisi, Tina nae aliitwa kituoni kwa
ajili ya kuhojiwa, alipofika alishangaa kuwakuta shemeji zake kituoni walipo
muona tina walijaribu kuficha sura zao lakini hawakuweza,Tina alihuzunika sana,
pale tu alipoambiwa shemeji yake ndie amemfanyia unyama wote ule. Tina aliogopa
sana akaangua kilio huku anasema, ni wewe kweli ? kwa nini laki umeamua
kunifanyia jambo baya Kiasi kile? Nimekukosea nini mimi? au nilifanya makosa
kuolewa na Ndugu yenu? kwani lakini mmekuwa wabaya kwangu? Mmenidhulumu mali za
mume wangu na mimi pia mnataka muniuwe? Kangomba alishikwa na aibu, alijikaza
lakini alishindwa akadondoka chini pu! Sunga nae alipata mshtuko kwa kuona mdogo
wake amedondoka, palepale na yeye alidondoka chini pu! Tina alishangaa akapatwa
na woga na huruma ulimjaa akasema, nimewasamehe
jamani sitaki mufe kwa ajili yangu, lakni wapi! Wote walipoteza maisha
palepale,Tina alilia sana akapoteza muelekeo, mahakama ilijaribu kumsaidia Tina
kupata mali zake lakini kumbe
vilishauzwa na shemeji zake, Tina alilia sana mwisho akaona amshukuru Mungu kwa
yote yaliyotokea.
SEHEMU YA TANO
Chiku
sasa amekua msichana mkubwa amemaliza elimu yake ya Msingi anasubiria majibu
ili aweza kujiunga na elimu ya sekondari. Kwa upande wake maisha yalikua magumu
kila kunapokucha, mama yake sasa ameacha kufanya biashara ya mkaa kwa sababu
imemuathiri kiafya imemsababishia ugonjwa wa kifua, hivyo hawezi tena kufanya
biashara hiyo. Vilevile hata kutembea kwa umbali mrefu hawezi tena, kifua
kikianza kumbana anakohoa hadi damu zinamtoka mdomoni. Chiku aliendeleza
biashara ya matunda na mbogamboga ambayo ingeweza kumsaidia katika matumizi
madogo madogo lakini haikumsaidia kwa kua pesa zote alizozipata ziliishia
kulipa kodi ya nyumba ambayo wanaishi.
Siku moja Tina alienda kwenye
mizunguko yake kama ilivyo ada yake kuuza matunda na mboga mboga wakati yupo
njiani alikutana na mvulana ambaye alisoma nae yule mvulana aliita Chikuuu! Chiku
akageuka kisha akasema waaooo! Hee! Umemaliza shule ndo umenenepa kiasi hiki?
Yule kijana aliyejulikana kwa jina la Jelia alimkejeli kwa kumwambia naona wewe
ndo umekua mrembo kama angle. Mmhh!! Ebu acha kunikejeli wewe, Chiku alimjibu
kwa sauti iliyojaa aibu. Chiku alisogea kwenye kivuli cha mti pembezoni kidogo
na barabara, na Jelia alisogea karibu ya Chiku kisha akamwambia majibu ya
mtihani yemetoka, katika Darasa letu tumefaulu watu watano tu! Chiku aliuliza
kwa shauku na mimi nimefaulu? Jelia alimjibu ndio umefaulu unatakiwa kuripoti
shule hivi karibuni, vipi na rafiki yangu Emma? Yeye hajafaulu Jelia alimjibu,
katika hao msichana ni peke yako. Chiku alifurahi sana ila alijua hatoweza
kwenda shule maana mama yake hakua na pesa za kumpeleka shule, Chiku alimwambia
jelia basi acha mimi nirudi nyumbani nikampe mama taarifa, wakaagana kwa furaha
isiyo na kifani. Chiku aligeuza na kupelekea nyumbani kwao, alipofika nyumbani
alimkuta mama yake imemuanza homa yake ya kifua, anakohoa kikohozi cha damu,
ameishiwa nguvu na anatapatapa mithili ya kuku anayetaka kutaga, mama!! Chiku
aliita kwa mshangao, akaangalia mkono wake akaona ana Shilingi elfu tatu tu za
kitanzania na ndani alikua na akiba ya Shilingi elfu kumi na tano ambayo ndio
pesa ya kulipa kodi ya nyumba, akawaza kisha akaona ni bora amuwaishe mama yake
hospitali, haraka akaita bajaji, tayari kwa kumpeleka mama yake hospitali,
punde si punde waliwasili hospitali haraka Tina alipelekwa katika chumba
maalumu na kuanza kupatiwa matibabu, ila kifua kilikua kimembana sana mpaka
akashindwa kupumua vizuri, Tina alimuomba Chiku aongee nae maneno mawili
matatu, Chiku aliwahi ndani akamkuta mama yake anapumua kwa shida sana, Chiku
alimwuliza mama yake, vipi hali yako? Tina alimjibu mwanae, mwanamgu nimekata
tama ya kuishi naona muda unasogea na hali inakua tete, siwezi kupona tena, ila
nakuomba uwe mwanamke jasiri, mtulivu, msikivu, mnyenyekevu na mwenye huruma
kwa kila mtu unayemjua na usiyemjua, mkubwa na mdogo, Chiku alilia sana huku
anamwambia mama yake, mama nimefaulu mwanao! Nahitajika kuripoti shuleni hivi
karibuni, Tina alizidi kupumua kwa shida sana kisha akamshika mwamawe mkono
palepale akapoteza maisha, Chiku alilia kwa uchungu wa hali ya juu, aliumia
sana, aliwaza ni nani ambae atamsaidia, nani ambae atamhurumia na ni nani ambae
atamshauri pale atakapopatwa na matatizo. Basi harakati za mazishi zikafanyika,
kutokana na ukarimu aliokua nao Tina katika uhai wake alizikwa na wanakijiji,
ilihali hakuwa na Ndugu hata mmoja katika kijiji kile ispokua mtoto wake tu!
Chiku alihuzunika alikosa amani katika maisha yake kila alipomkumbuka mama yake
alikosa furaha na pale aliporudisha mawazo yake nyuma alimkumbuka baba yake
kipenzi bwana Alfni, alikosa furaha japo kua majirani walijitahidi kumfariji
ili aweze kusahau yale yaliyotokea lakini chiku katu hakuweza kurudisha furaha
yake ya asili. Walimu wa shule ya msindi aliyosoma walimpa moyo pia wanafunzi
ambao alihitimu nao Darasa la saba walimpa moyo, ila Chiku hakurudi katika hali
yake ambayo watu walizoea kumuona.
SEHEMU YA SITA
Mwezi mmoja sasa tangu Tina ameaga
dunia, maisha ya chiku yalienda ndivyosivyo kila jua linapochomoza aliona bora
ya jana kuliko leo, alipewa taarifa kua amechaguliwa kujiunga na shule ya
sekondari Kazimoto iliyopo wilayani Masasi lakini hakua na pesa
zitakazomwezesha kuendelea na masomo hayo, alijaribu kuomba msaada katika
sehemu tofauti, waalimu nao walijitahidi kutafuta wafadhili ambao wangeweza
kumsomesha yatima huyu lakini jitihada zote ziligonga mwamba, mpaka wanafunzi
wote wakapelekwa mashuleni na wazazi wao, muda wa wanafunzi kuripot shule
ukaisha na habari ya Chiku kusoma zikaishia hapo.
Chiku aliendeleza biashara yake ya
mbogamboga na matunda kijiji kizima alijulikana kwa ujasiri na ukarimu wake
watu walimpenda sana, alikua na kauli nzuri kwa wateja wake vilevile alimheshimu
kila mmoja mwenyeji na mgeni wakubwa kwa wadogo wanawake kwa wanaume, maisha
yaliendelea hivyo hivyo akipata anakula akikosa analala.
Siku moja Chiku hakwenda kwenye
biashara zake alipumzika nyumbani, akafanya usafi wa chumba chake pamoja na
Mazingira yaliyozunguka nyumba ile, alipomaliza akaandaa chakula akala, wakati
anakula alikumbuka malezi ambayo marehemu mama yake alimpa alijikuta anatokwa
na mchozi, ghafla mlango uligongwa, aliogopa kisha akakumbuka kilichomkuta mama
yake, lakini alijipa moyo kwa kua ilikua mchana kweupe. Akafungua mlango,
akashangaa kuona vijana wawili wameingia ndani na yeye akasukumizwa ndani kisha
vijana wale wakafunga mlango. Walimvamia na kumfunga kitambaa cheusi usoni
kijana mmoja alimziba mdomo Chiku mwengine akaanza kumvua nguo, chiku alijaribu
kujitoa mikononi mwa wawili wale lakini hakuweza, kijana mmoja akamwambia
mwenzie anza alafu mimi nitafuatia, akafungua zipu ya suruali yake, yele
aliyemziba mdomo Chiku akaona mwenzie anachelewa akamwachia, ili aanze yeye,
palepale Chiku akapata mwanya, haraka akotoa kitambaa usoni, karibu yake
kulikua na chupa ya soda akaishika kwa nguvu akamrushia mmoja wao ikampiga
kichwani, kijana aliyebakia alisahau yaliyomleta pale akaanza kushughulika na
mwenzie aliyezimia kwa kipigo alichopokea kutoka kwa Chiku. Chiku alichukua
kipande cha chupa ile iliyovunjika akamchoma nayo kijana Yule katika jicho
lake, alipiga makelele kama paka aliyepigwa kwa kosa la kuiba kitoweo, Chiku
aliogopa akachanganyikiwa na hakuamini kama mikono yake ndio imefanya tukio
lile. Haraka alivaa nguo akachukua begi lake la nguo na kipochi chake chenye
fedha akaangalia nje akagundua hakuna mtu akatimua mbio mpaka stendi ya mabasi
alipofika hakuchelewa aliingia ndani ya gari na gari ilikua tayari imeshapakia
abiria ikachapa mwendo, yumo ndani ya gari machozi yalimbubujika, abiria wote
waliokua ndani ya gari lile walimkodolea macho lakini yeye hakujali. Lakini aliwaza wapi atakwenda kufikia, ili
hali yeye hajawahi kwenda mjini hata siku moja na hana anayemfamu hana Ndugu
wala rafiki, lakini alijiamini na akakumbuka wosia aliopewa na marehemu mama
yake kua siku zote awe jasiri na mwenye kujiamini.
Ilipofika saa moja na nusu usiku
gari liliwasili jijini Dar es salaamu abiria walishuka Chiku naye akashuka kila
mtu aliingilia upande wake wapo waliokodisha taksi wengine bajaji na wengine
bodaboda wawafikishe majumbani mwao. Chiku hakuelewa aingilie wapi, alishangaa
shangaa tu mara aangalie huku mara kule akakiona kinjia kidogo akasema subiri
nifate njia hii, wakati anafuata njia ile kuna vibaka wawili wakawa wanamfuata
kwa nyuma, Chiku alihisi kuna watu wanamfuata aliongeza mwendo akagundua kua na
wao wanaongeza mwendo, Chiku alitimua mbio kule anakoelekea kulikua na barabara
kubwa ya magari, ile anataka kuvuka barabara kuna gari lilikua linatembea kwa
kasi likamzoa yeye na begi lake begi lake la ngua likarukia mtaroni dereva wa
gari alifunga breki ghafla wakashuka mwanamke na mwanaume, wakamnyanyua
wakamuweka ndani ya gari wakamuwahisha hospitalini. Chiku alipatiwa matibabu
mpaka akapona, akawa katika hali nzuri, huku kijijini taarifa za kutoroka Chiku
zilisambaa na wale vijana wawili waliotaka kumnajisi Chiku walipoteza maisha na
hakuna aliyehangaika kuhoji juu ya vifo vyao kwa sababu walijulikana kwa tabia
chafu.
SEHEMU YA SABA
Baada ya chiku kupona alichukuliwa
na wawili wale moja kwa moja mpaka nyumbani kwao, walipofika wakamkaribisha
vizuri, akapewa chakula, alipomaliza aliwashukuru kwa yale yote waliyomsaidia,
baadae utambulisho ulianza, mimi nimaitwa Toni na huyu ni mke wangu anaitwa
Janeth sijui wewe unaitwa nani? Naitwa Chiku, unaishi wapi? Toni aliuliza Chiku
alijibu kwa unyonge naishi…………. Akasita kidogo kisha akaanza kutokwa na machozi
huku anasema ni historia ndefu sana, aliwasimulia yote yaliyomkuta hadi kufikia
hatua ya yeye kukimbilia mjini. Toni na Janeth walimhurumia sana kwa yale
ambayo yamemkuta hali ya kua bado ni mtoto mdogo. Wakamuahidi kumsaidia kwa
yale ambayo yako ndani ya uwezo wao, walimnunulia nguo nzuri na viatu vizuri na
wakamtafutia shule akajiunga kidata cha kwanza.
Chiku ni mtoto ambae alikua na
nidhamu kwa walezi wake pamoja na waalimu wake, furaha ilirejea taratibu, Toni
na Janeth walijitahidi kumpa Chiku mahitaji yote ambayo yanahitajika kwa mtoto,
Chiku nae alijitahidi kuwa mtiifu kwa walezi wake wapya.
Kutokana na maisha mazuri aliyoishi
Chiku kwa muda ule, urembo wake ulijidhihirisha alikua ni mrefu wa wastani
mwenye umbo namba nane, pua yake ndefu kidogo na macho yake yalikua ni makubwa
kidogo ya uduara yalimvutia kila aliyemuangalia nguo za shule zilimkaa vizuri
hadi wasichana wenzie wakamuonea wivu, wavulana wengi walijipitisha karibu ya
Chiku lakini Chiku alikua kafundwa akafundika hakuwa na tabia chafu ambazo
wasichana wengine walikua nazo. Alijituma kadiri awezavyo katika masomo yake
waalimu walimpenda sana Chiku.
Siku moja wakiwa darasani, mwalimu
alikua anafuindisha somo la hisabati, Chiku alikua makini sana kumsikiliza
mwalimu, kuna mvulana mmoja aliyeketi karibu na Chiku alionekana kumuangalia
sana binti yule kwa jicho la wizi, mwalimu akagundua akaita wewe kijana njoo
utufanyie swali moja hapa ubaoni, kijana alishtuka ila alijikaza akanyanyuka na
kwenda ubaoni kujaribu kufanya swali aliloambiwa alifanye. Kwa sababu ya
kutokua makini kusikiliza alishindwa kufanya swali, Chiku alonyoosha mkono
ishara ya kutaka kwenda kumsaidia yule kijana, mwalimu alimpa nafasi Chiku,
Chiku alinyanyuka na kuelekea ubaoni akalifanya swali vizuri na kwa usahihi
wake, very good mwalimu alimpongeza Chiku na akawashauri wanafunzi wengine
waige tabia na mienendo ya Chiku. Wakati
chiku anaelekea kwenye kiti chake mwalimu alijikuta anamuangalia Chiku kwa umbo
lake zuri ambalo amejaaliwa na mungu mwisho akasema someni….. someni…. Someni saana
wanafunzi kisha akaondoka
Kengele ya kurudi nymbani iligongwa,
kama kawaida ya Chiku kengele ikisikika tu huwa hana mambo mengi anayoyafanya
zaidi ya kuchukua begi lake la madaftari na kwenda kumsubiria Toni amfuate ili amrudishe
nyumbani, wakati anamsubiria Toni aje na usafiri kuna kijana mrefu ambae alikua
kidato cha tatu alimsogelea Chiku kisha akamsalimia, Afternoon miss, Chiku
alimjibu Afternoon how are you? Yule kijana alianza kuropoka kwa majina
ninaitwa Kilian John Mgalula ni kaka mkuu katika shule hii ya St. Joseph, chiku
alimjibu Oooh! Nimefurahi kukufahamu, punde si punde Toni alifika na gari yake
Chiku akaingia ndani ya gari na kumuacha Yule kijana mdomo wazi, Toni aliwasha
gari hao wakaondoka. Kijana alijihisi amedharauliwa ile anageuza shingo yake tu
macho kwa macho akakutana na msichana anayeitwa Anna alikua amekasirika kisha
akasema Kilian umekosa nini wewe mwanaume mpaka umfate bint mdogo wa kidato cha
kwanza, mwangalie mvulana umekosa haya wewe!! Au kwa kua mimi baba yangu hana
gari, ujue Kilian unauumiza moyo wangu. Kwa dharau kilian alimjibu Anna kuanzia
leo usinijue, mwanamke gani wewe mfupi kama kipande cha sabuni, mwanamke
mshamba mshamba kaa mbali na mimi, kisha huyo akaondoka. Anna alikaa chini
taratibu akalia kwa uchungu baadae alinyanyuka akaondoka.
Chiku alionekana kua ni
mtoto bora, mtiifu, Mwaminifu na mkarimu kila kunapokucha, waalimu walizidi
kuvutiwa na tabia za Chiku, walezi wake pia walimwamini na wakamwona kama mtoto
wao wa kumzaa. Chiku ni msichana ambaye anajituma kila anapoamka asubuhi
anasafisha chumba chake, anaosha vyombo na kudeki nyumba nzima, akimaliza
anajiandaa kwa ajili ya kuwahi shule. Anapokua shule hapendi kujichanganya na
makundi mabaya ambayo yatamharibia maisha. Siku moja Chiku alikua ameketi chini
ya mti wenye kivuli kizuri uliopo katika Mazingira ya shule akiwa amefunua
kitabu chake cha tamthilia anasoma, ghafla aliona kundi la wasichana wapatao
saba wa kidato cha tatu wanakuja pale alipo, walipofika tu bila ya salaam
wakaanza kumshambulia kwa maneno machafu na matusi, mmoja wao aliyejulikana kwa
jina la Anna alimwambia Chiku, wewe mtoto kaa mbali na Kilian, usipofanya hivyo
utanijua mimi ni nani? Akampokonya kitabu akakichana chana akamrushia usoni,
Chiku hakusema chochote alikaa kimya, mmoja wao akasema yaani huyu mtoto
anaonekana ni kiburi sana mwangalie kwanza macho yake yalivyo. Wasichana wale
waliondoka, Chiku alilia kwa hasira lakini hakupenda ugomvi, sio kama
alishindwa kuwatemea maneno machafu, lakini kutokana na nidhamu aliyonayo
alitulia kimya, wakati tukio lile likiendelea Kilian alikua anashuhudia kile
kilichotokeo alijibanza kwenye ukuta wa Darasa na akashuhudia yote. Kilian
alimuhurumia sana Chiku, akaona aende moja kwa moja hadi kwenye ofisi ya
nidhamu akatoe taarifa, alipofika alimkuta mwalimu ameketi kisha akamueleza
yote, mwalimu alisema nyie ndio viongozi ambao tunawahitaji katika shule yetu.
Punde si punde kengele ya dharula ikagongwa wanafunzi wote wakakusanyika
paredi, kaka mkuu ambaye ni Kilian aliwaamuru wanafunzi wanyamaze kwan kuna
tangazo kutoka kwa mwalimu wa nidhamu. Mwalimu wa nidhamu alianza kwa
kuwasalimia wanafunzi kisha akasema wafuatao wapite mbele! Akaita majina ya
wasichana saba kisha akawaambia wapige magoti mbele ya wanafunzi wenzao, kisha
akamuomba Chiku nae aje mbele, Chiku aliogopa akaanza kububujikwa na machozi,
wakati anaenda mbele wanafunzi wote walimkodolea macho, waalimu nao hawakuweza
kuyazuia macho yao yasimtazame Chiku, walimuangalia mtoto jinsi anavyotembea ,
na umbo lake jinsi lilivyokua la kipekee na sura yake ilimvutia kila
aliyemwangalia, alipofika mbele, mwalimu wa nidhamu alisema hawa asichana saba
wamemshambulia kwa matusi binti huyu ambaye hana hatia, wanafunzi wote
walishangaa, Chiku nae alishangaa taarifa zimefikaje kwa mwalimu? Hivyo basi
tutawatandika fimbo tatu tatu kila mmoja ili iwe funzo kwa wengine na mwisho
tutaweapa barua waendenazo kwa wazazi wao. Mwalimu Yule alichukua fimbo
akawatandika kama alivyosema na kisha akawapa barua, hao wakaondoka. Kuanzia siku
hiyo wanafunzi walimuheshimu Chiku hakuna ambaye alitaka kumuonea, kwa upande
wake Chiku siku hiyo hakua na amani hata kidogo, hata pale Toni alipomfuata
aligundua kuwa Chiku hakuwa na furaha. Walipofika nyumbani, Toni na Janeth
walijaribu kumuuliza Chiku kwa nini hana furaha? Akawarleza yale yote
yaliyotokea. Toni na Janeth walijaribu kumfariji Chiku, na hakuchukua muda
akarudi katika hali yake ya kawaida.
SEHEMU YA TISA
Katika maisha ya shule Chiku
alikumbana na changamoto nyingi sana lakini alijitahidi kupambana nazo, baadhi
ya waalimu wenye tabia chafu walijaribu kumrubuni Chiku, lakini Chiku alikua na
malengo yake. Alipokua kidato cha pili alishika nafasi ya kwanza ya kwanza
katika mkoa wa Dar-es-Salaam, shule ilimzawadia kwa kuipa shule hiyo sifa
nzuri, lakini pia alipata Zawadi nyingi kutoka mkoani, walezi wake pia walipewa
Zawadi kwa matunzo mazuri ya mtoto wao, aliingia kidato cha tatu akiwa na
furaha tele moyoni. Mara kwa mara waalimu walimuomba Chiku awashauri wanafunzi
wenzake katika masomo, Chiku alijaribu kupanga ratiba yake vizuri ili aweze
kuwasaidia wenzie, lakini alihitaji kupata muda wa ziada ambao angeutumia
kujisomea mwenyewe maana muda mwingi aliutumia kuwasaidia wenzie. Chiku
aliwaomba walezi wake abakie shule kwa muda wa masaa mawili pale ambapo wenzie
wanarudi nyumbani ili aweze kujisomea, kwa kua walezi wake hawakua na shaka nae
aliruhusiwa lakini walimshauri awe makini. Chiku alifurahi kuona walezi wake
wanamuamini na kujali anachokihitajia, siku moja Chiku alikua amebakia darasani
peke yake wakati wanafunzi wote wamekwishaondoka, akajikuta amemkumbuka
marehemu mama yake, taabu na shida zote alizopitia wakati yu mdogo akajikuta
atabubujikwa na machozi, wakati Chiku analia kuna mwalimu alikua anapita nje
akahisi kuma kuna sauti inatoka ndani ya Darasa, ikibidi aangalie ni nani
ambaye yumo ndani, alipofika alishangaa kumuona Chiku ambaye alikua anamtafuta
na kumsaka kwa muda mrefu, taratiibu akaingia kisha akamziba macho, Chiku
aliogopa sana, Yule mwalimu akasema usiogope ni mimi, Chiku alipogeuka
alikutana macho kwa macho na Yule mwalimu, Chiku alichukia akasema, mwalimu kwa
nini lakini haujiheshimu, Yule mwalimu alimjibu hivi mpaka leo unaniita mwalimu, niite jina langu
bwana, mimi ninaitwa Sheby. Mmh !! Chiku aliguna kisha akakusanya madaftari
yake na kuyaweka ndani ya begi akanyanyuka na kuanza kuondoka, mwalimu Shebi
alimshika mkono Chiku kisha akachomoa kitita cha fedha mfukoni akampa kisha
akamwambia nifikirie. Chiku alizipokea zile fedha kisha akamrushia usoni,
akamwambia thamani ya utu wangu hailingani na hivyo vijisenti vyako kisha huyo
akaondoka.
Mwalimu alihisi amedharaulika kisha
akajilaumu ni kwa nini alimfuata binti Yule, lakini alijisemea kimoyomoyo
nitampata tu! Nitafanya kila mbinu hadi nipate ninachokitaka, walikuapo wengi
wanaofanana na yeye lakini leo wako wapi mbona nilishawapata? Nitampata tu hata
kama isiwe mwaka huu. Chiku alielekea barabarani dakika chache tu na Toni nae
alimfuata, kisha aliingia kwenye gari hao wakaondoka, Sheby nae hakuchelewa
akaondoka.
SEHEMU YA KUMI
Mwalimu Sheby hakuchoka kumfuatilia
Chiku, alijitahidi kumpa maneno ya kila aina lakini Chiku alikua mgumu kama
kisiki cha mpingo, aliyasikiliza maneno yake lakini hakuyazingatia hata kwa
udogo wa mdudu Chungu. Lakini mwalimu sheby hakukoma, Siku moja kulikua na
kikao baina ya waalimu na wanafunzi wote wa St. Joseph. Cha kushangaza waalimu
wote waliende kwenye kikao na wanafunzi wote walikua kwenye kikao ila mwalimu
Sheby tu alibakia ofisini. Kwa mbali alimwona mwanafunzi akielekea waliko
wenzake, akamwita kisha akamwambia naomba ukaniitie Chiku mwambie anaitwa
katika ofisi ya taaluma, yule mwanafunzi alifikisha taarifa kama alivyoagizwa.
Chiku alifikiri kwa muda kidogo ni kipi aliitiwa katika ofisi ya taaluma,
alikua na wasiwasi wa hali ya juu kisha akanyanyuka na kuelekea kule alipoitwa,
alipofika aligonga mlango, mlango ulifunguliwa akaingia ndani, alipoingia tu
mwalimu Shebi alifunga mlango na funguo akaweka mfukoni, Chiku akashangaa kisha
akauliza mwalimu mbona unafunga mlango? Mwalimu Shebi alitabasamu kisha akasema
ina maana wewe hujui, bila kuchelewa mwalimu Yule alimshika Chiku mabega
akamgandamiza ukutani kisha akamwambia kwa muda mrefu nilikua nakutafuta!
Nafasi hii siamini kama leo nimeipata, Chiku alitetemeka kama amepigwa shoti ya
umeme, akaseme mwalimu mimi sihitaji unachohitaji wewe naomba uniache niondoke,
mwalimu shebi alitabasamu huku anaupapasapapasa mgongo wa Chiku, Chiku
alihamaki akapiga kelele lakini wapi kelele zake ziliishia ndani ya ofisi ile
tu na nje haikutoka hata herufi ya sauti kwa kua ofisi ile ilikua na madirisha
ya vioo. Mwalimu Shebi alijaribu kutaka kumnajisi mwanafunzi wake lakini
mwanafunzi pia hakua nyuma Kutumia ujasiri alonao kujinasua katika mtego ule.
Ama kweli mapenzi ni upofu, ububu na upofu, mwalimu hakuona kua yupo ndani ya
ofisi hakusema neno lolote na wala hakusikia kilio na kelele za Chiku
alichanganyikiwa akanza kumvua Chiku nguo kwa nguvu lakini Chiku alijitahidi
kumzuia, mwalimu Shebi alivuta shati la Chiku kwa nguvu hadi akalichana
akabakiwa na kitopu ambacho kimemsitiri kifua chake, looh! Mwalimu alizidi
kuchanganyikiwa alipoona kifua cha Chiku, Chiku alikasirika akamsukuma mwalimu
mpaka akajigonga kwenye meza ya kioo ambayo ilikuwa nyuma yake na meza
ikapasuka, mwalimu Yule alipoteza fahamu palepale, Chiku aliogopa na alilia
sana huku anasema, kwa nini mimi kila siku nakua kwenye matatizo, nina kosa
gani mimi, nimewakosea nini watu hadi wananisababishia matatizo? Alipoangalia
dirishani aliwaona waalimu wanakuja kwa mbali, akajaribu Kufungua madirisha ili
aondoke akashindwa, akakumbuka kua funguo zilikua kwenye mfuko wa suruali ya
mwalimu, haraka akamsogelea mwalimu na kuchukua funguo, wakati anatoa mkono wake
mfukoni akajikata na kipande cha kioo ambacho kilikua kimevunjika kwenye ile
meza, ila hakuhisi maumivu, akafungua mlango haraka, ile anatoka nje tu
akakutana ana kwa ana na mwalimu mkuu pamoja na waalimu wengine, kwa woga na
hofu aliyokua nayo akapata mshtuko mkubwa akadondoka chini pwaaaa! Kama mzigo palepale akapoteza fahamu,
waalimu walishangaa, walopoangalia kwenye ule mlango ambao Chiku ametokea
wakaona mtu amelala waliposogea karibu zaidi walishangaa kumuona mwalimu Shebi
ameangukia meza na meza imevunjika vunjika, haraka wakapiga simu polisi, polisi
wakaja. Wakachunguza eneo la tukio hawakugundua kitu chochote, Chiku na mwalimu
Sheby wakawahishwa hospitali. Taarifa zilizagaa kila kona ya jiji kwa muda
mchache kwa Kutumia televisheni, redio magazeti na mitandao ya kijamii. Toni na
Janeth walipopata taarifa haraka wakaingia kwenye gari lao kuwahi sehemu ya
tukio, wakati wapo njiani gari ilikua mwendo kasi sana ili kuwahi eneo la
tukio, ghafla gari ikaacha njia na kugonga mti uliopo pembezoni mwa barabara
pale pale gari likapinduka juu chini na wote wawili wakapoteza maisha. Waalimu
walipata taarifa ya ajali waliyoipata walezi wake Chiku, muda ule ule daktari
akatoa taarifa kuwa Chiku ameaga dunia. Lakini mwalimu yupo hai, waalimu
walipata pigo kubwa sana kwa kuondokewa na mwanafunzi ambae ndio jicho lao.
Madaktari walikua makini sana na
mgojwa aliyebakia maana wakimpoteza yeye ushahidi wote unaweza ukapotea.
Madaktari bingwa wanaotoka hospitali tofauti jijini Dar-es-Salaam waliunganisha
ujuzi wao ili kunusuru uhai wa mgojwa Yule, wiki mbili mbele mwalimu Sheby
alipata nafuu, waandishi wa Habari hawakucheza mbali kwasababu walikua
wanahitaji kumuhoji mwalimu yule. Baada ya afya ya mwalimu yule kukaa vizuri
hawakuchelewa wakampeleka kituoni kwa ajili ya mahojiano ya kina juu ya tukio
lililotoke, walipojaribu kumuhoji alikana kutoa Ushirikiano na wapelelezi wale,
akapelekwa chumba cha adhabu bila kujali kua ametoka hospitali muda mfupi
uliopita, baada ya kuona adhabu zimezidi mwalimu Sheby akasema yote
yaliyotokea. Hivyo mwalimu sheby alifikishwa mahakamani na hakimu akamuhukumu
kifungo cha maisha kwa kosa la kusababisha kifo cha mwanafunzi.
Waalimu waliwanasihi wanafunzi
waliobakia shule waige mfano wa Chiku kwani ni msichana jasiri sana na amekufa
kishujaa. Picha za Chiku zilisambaa magazetini na jiji lote lilipata taarifa
kuhusu ujasiri wa binti Chiku, Ama kweli kizuri hakidumu.